Picha ya Oktoba,
2009: (Kutoka kushoto) Mchoraji kutoka Ghana, marehemu Frank Odoi, Daryl Cagle
wa Marekani na mimi.
Nilizipokea kwa mshtuko mkuu habari za kifo cha mchoraji
wa ki-Ghana aliyekuwa akiishi na kufanyia shughuli zake nchini Kenya, Bw. Frank Odoi, kutokana
na ukweli kuwa kifo hicho, kilichotokea kwa ajali ya gari, kilikuja siku moja
tu baada ya kuwa tumewasiliana kwa simu akiwa Nairobi.
Nilimfahamu Odoi, ambaye alifahamika sana miongoni mwa
wachoraji wakongwe wa michoro ya machapisho nchini Tanzania, katikati ya miaka
ya '90 jijini Dar Es Salaam. Wakati huo katuni zake ikiwemo ya ‘You
drive me crazy’ zikiwa zinachapishwa katika baadhi ya machapisho hapa
nchini. Katika mfululizo wa katuni hizo za You drive me crazy, Bw. Odoi alikuwa
akisawiri mitafaruku inayotokea katika uendeshaji na usalama barabarani. Leo,
mauti yake yamesababishwa na ajali za barabarani alizokuwa akizisawiri!
Lakini ilikuwa ni wakati wa Tamasha la pili la utamaduni
wa Mwafrika (Pan African Cultural Festival) lililofanyika Algiers, Algeria kwa
majuma matatu, Julai, 2009, ndipo nilipokuja kujenga urafiki na mchoraji huyu mcheshi
na rafiki.
Katika zaidi ya wachoraji 20 tulioalikwa kushiriki katika
tamasha hilo, lililojumuisha sanaa na tamaduni anuwai za kiafrika, ni mimi,
Odoi na mchoraji wa kinaijeria anayeishi
Uingereza, Tayo Fatunla, ndio pekee tuliotoka nchi zinazozungumza kiingereza (Kimataifa,
Tanzania huwekwa miongoni mwa nchi zinazozungumza kiingereza). Hivyo tulikuwa karibu sana. Hasa ukizingatia,
Tayo alichelewa kuwasili.
Ni wakati huu, aliponipatia na kutia saini kwa ajili yangu nakala ya
kitabu cha komiki yake maarufu ya Akokhan.
Nilikutana tena na Odoi,
Oktoba, mwaka huo huo jijini hapo hapo Algiers, safari hii tukiwa
tumealikwa kushiriki katika Maonyesho ya kimataifa ya komiki. Toka wakati huo
mimi na Odoi hatukupotezana. Tuliwasiliana sana kwa barua pepe na aliniwezesha
kuchora katuni kadhaa katika machapisho ya jarida la Pop Ed linalochapishwa
na UNFPA nchini Kenya.
Kwa karibu mwaka mzima sasa, Mimi na Odoi hatukuwa
tumewasiliana. Bila shaka, kutokana na harakati za kimaisha, lakini Alhamisi ya
19/04/2012, siku mbili kabla ya kifo chake, Odoi aliwasiliana nami na safari
hii kwa mara ya kwanza ‘akivunja’ utaratibu wa kuwasiliana kwa barua pepe.
Alinipigia!
Tuliongea sana na akaahidi kunipigia tena siku inayofuata
kuhitimisha kilichofanya anipigie. Ijumaa (yaani siku moja kabla mauti ya
ghafla kumfika!), Odoi, ka’ alivyoniahidi, alipiga na kunitaarifu kuwa pana
barua pepe atanitumia punde na akanitaka nimpe mrejesho pindi nitakapokamilisha
yaliyomo katika barua-pepe hiyo.
Kila kitu kilikwenda sawa! Saa kumi kasorobo –kwa mujibu
wa kumbukumbu ya simu yangu (simu ambayo niliitazama tena mara baada ya kupata
taarifa ya mauti yake ya ghafla)-, nilimpigia kumpa mrejesho na kisha tukaongea
kidogo mambo mengine ya kikazi.
Katika ngoma ya sikio langu la kushoto, sikio ambalo kwa
kawaida ndilo n’nalolitumia kusikilizia simu, ningali n’naikumbuka sauti ya Odoi
ikihitimisha mazungumzo nami kwa kuniambia ‘Okay, Popa!’
Isingeweza kusambaa kichwani mwangu, kwamba nilikuwa
ninamsikia Frank Odoi kwa mara ya mwisho! Kwamba siku inayofuata (Jumamosi,
21/04/2012), katika moja ya barabara za Nairobi, ajali ya gari, ingekuja kukatisha, ghafla, maisha ya
mchoraji huyu mwenye kipaji, bashasha, mahoka kemkem na aliyekipenda kinywaji
chake!
Frank Odoi, nenda kapumzike. Kwa tuliosalia na
kukufahamu, utaishi fikrani mwetu na kazi zako zitabaki kuwa kumbukumbu ya kudumu ya ulichoifanyia jamii yako.
No comments:
Post a Comment