Sunday, April 29, 2012

Kapumzike Frank Odoi


Picha ya Oktoba, 2009: (Kutoka kushoto) Mchoraji kutoka Ghana, marehemu Frank Odoi, Daryl Cagle wa Marekani na mimi.

Nilizipokea kwa mshtuko mkuu habari za kifo cha mchoraji wa ki-Ghana aliyekuwa akiishi na kufanyia shughuli zake nchini Kenya, Bw. Frank Odoi, kutokana na ukweli kuwa kifo hicho, kilichotokea kwa ajali ya gari, kilikuja siku moja tu baada ya kuwa tumewasiliana kwa simu akiwa Nairobi.

Nilimfahamu Odoi, ambaye alifahamika sana miongoni mwa wachoraji wakongwe wa michoro ya machapisho nchini Tanzania, katikati ya miaka ya '90 jijini Dar Es Salaam. Wakati huo katuni zake ikiwemo ya  ‘You drive me crazy’ zikiwa zinachapishwa katika baadhi ya machapisho hapa nchini. Katika mfululizo wa katuni hizo za You drive me crazy, Bw. Odoi alikuwa akisawiri mitafaruku inayotokea katika uendeshaji na usalama barabarani. Leo, mauti yake yamesababishwa na ajali za barabarani alizokuwa akizisawiri!

Lakini ilikuwa ni wakati wa Tamasha la pili la utamaduni wa Mwafrika (Pan African Cultural Festival) lililofanyika Algiers, Algeria kwa majuma matatu, Julai, 2009, ndipo nilipokuja kujenga urafiki na mchoraji huyu mcheshi na rafiki.

Katika zaidi ya wachoraji 20 tulioalikwa kushiriki katika tamasha hilo, lililojumuisha sanaa na tamaduni anuwai za kiafrika, ni mimi, Odoi na mchoraji wa kinaijeria  anayeishi Uingereza, Tayo Fatunla, ndio pekee tuliotoka nchi zinazozungumza kiingereza (Kimataifa, Tanzania huwekwa miongoni mwa nchi zinazozungumza kiingereza).  Hivyo tulikuwa karibu sana. Hasa ukizingatia, Tayo alichelewa kuwasili.

Ni wakati huu, aliponipatia na kutia saini kwa ajili yangu nakala ya kitabu cha komiki yake maarufu ya Akokhan.

Nilikutana tena na Odoi,  Oktoba, mwaka huo huo jijini hapo hapo Algiers, safari hii tukiwa tumealikwa kushiriki katika Maonyesho ya kimataifa ya komiki. Toka wakati huo mimi na Odoi hatukupotezana. Tuliwasiliana sana kwa barua pepe na aliniwezesha kuchora katuni kadhaa katika machapisho ya jarida la Pop Ed linalochapishwa na UNFPA nchini Kenya.

Kwa karibu mwaka mzima sasa, Mimi na Odoi hatukuwa tumewasiliana. Bila shaka, kutokana na harakati za kimaisha, lakini Alhamisi ya 19/04/2012, siku mbili kabla ya kifo chake, Odoi aliwasiliana nami na safari hii kwa mara ya kwanza ‘akivunja’ utaratibu wa kuwasiliana kwa barua pepe.

Alinipigia!

Tuliongea sana na akaahidi kunipigia tena siku inayofuata kuhitimisha kilichofanya anipigie. Ijumaa (yaani siku moja kabla mauti ya ghafla kumfika!), Odoi, ka’ alivyoniahidi, alipiga na kunitaarifu kuwa pana barua pepe atanitumia punde na akanitaka nimpe mrejesho pindi nitakapokamilisha yaliyomo katika barua-pepe hiyo.

Kila kitu kilikwenda sawa! Saa kumi kasorobo –kwa mujibu wa kumbukumbu ya simu yangu (simu ambayo niliitazama tena mara baada ya kupata taarifa ya mauti yake ya ghafla)-, nilimpigia kumpa mrejesho na kisha tukaongea kidogo mambo mengine ya kikazi.

Katika ngoma ya sikio langu la kushoto, sikio ambalo kwa kawaida ndilo n’nalolitumia kusikilizia simu, ningali n’naikumbuka sauti ya Odoi ikihitimisha mazungumzo nami kwa kuniambia ‘Okay, Popa!’

Isingeweza kusambaa kichwani mwangu, kwamba nilikuwa ninamsikia Frank Odoi kwa mara ya mwisho! Kwamba siku inayofuata (Jumamosi, 21/04/2012), katika moja ya barabara za Nairobi, ajali ya gari, ingekuja kukatisha, ghafla, maisha ya mchoraji huyu mwenye kipaji, bashasha, mahoka kemkem na aliyekipenda kinywaji chake!

Frank Odoi, nenda kapumzike. Kwa tuliosalia na kukufahamu, utaishi fikrani mwetu na kazi zako zitabaki kuwa kumbukumbu ya kudumu ya ulichoifanyia jamii yako.

No comments: