Thursday, December 9, 2010

Tanzania!

Ghafla, nishati ya umeme inaendea kuwa bidhaa adimu. Miaka 49 ya uhuru inashuhudia pungufu ya asilimia 10 ya watu wetu ndio pekee wanaoipata nishati hii, napo si kwa uhakika na wala hawana mamlaka nayo (hujui ni muda gani umeme utakatika!) Binafsi, nimesitisha matumizi ya jiko langu la umeme. Kisa?, Umeme umepata kukatika zaidi ya  mara tatu nikiwa katika harakati za kuliandalia tumbo ridhiko.
Ukiitazama ramani ya bara la Mama yangu, Afrika, vyanzo vikubwa vya maji vimetamalaki katika nchi nilipo! Lakini maji yaliyo safi na salama kwa wote ni hadithi endelevu isiyo na ukomo! Na tena,  kama vile haitoshelezi, kilimo chetu kingali kinategemea misimu ya mvua. Bob Marley ananikumbusha katika Rat race: ‘Katika mahali palipo na wingi wa maji, mpumbavu ana kiu!’
Hivi ni nini kinachoniongoza kuandika haya?  Taifa langu, Tanzania, liko katika kumbukumbu ya miaka 49 toka liwe taifa 'huru!' Wakati viongozi wangu wakuu WAMESHEREHEKEA sikukuu hii kwa mbwembwe kama ada, mimi ‘mpiga kura wao’na mzalendo azizi, nasikitika kusema, NIMEIADHIMISHA tu!

Ningali nalitakia taifa langu baraka njema! Baba, Mungu Mkuu, tubariki!

No comments: